Listening to General Secretary Bankmoon addressing delegates from different countries on the theme of session

Having a lunch with other delegates from different countries day one at UN Geneva-Switzerland(Europe)

The storm ended in 2012. It was the day unspeakable, and the joy unforgettable at Chimwaga Hill Conference: The University of Dodoma-UDOM

With special attention while taking photos at American Embassy in Nairobi Kenya

With the smiling face in Nairobi Kenya at American Embassy :From the left is Dannilo from Mozambique, Anderson from Tanzania, Dr.Katabaro-Tz, and the blogger in the right side Dr.Msoline

Friday, 13 January 2017

Migogoro ya ardhi itafutiwe ufumbuzi wa kudumu

Migogoro ya ardhi itafutiwe ufumbuzi wa kudumu

KWA sasa imekuwa kama vile ni wimbo wa taifa kusikia migogoro ya wakulima na wafugaji wakigombea ardhi. Hata hivyo huo ni mmoja tu kati ya migogoro mingi inayohusiana na ardhi.

Nchini Tanzania kumekuwapo na migogoro mingi hususani katika kugombea maeneo ya kilimo, malisho ya wanyama, maji n.k.

Baadhi ya migogoro hiyo imetatuliwa kwa njia ya amani na mingine imeshindikana na kusababisha mauaji ya kinyama kama ambavyo imekuwa ikijitokeza katika Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro na hata Kiteto mkoani Manyara ambako watu 15 waliuawa kwa mpigo katika makabiliano ya aina hiyo mwaka 2014.
Nilikuwa mmoja wa wawakilishi wa asasi za kiraia zilizokwenda kuchunguza mgogoro wa ardhi uliosababisha mauaji wilayani Mvomero mwaka 2013. Taasisi mratibu wetu ilikuwa ni taasisi ya Tanzania Land Alliance (TALA).

Lakini pia nilipata nafasi ya kutembelea mikoa yote nchini Tanzania Bara na Zanzibar. Baadhi ya mikoa niliitembelea katika safari zangu za binafsi, na mingine kama ilivyokuwa Morogoro na Pwani ni kwa ajili ya kufuatilia migogoro ya ardhi.

Sehemu nyinginezo nilizotembelea nikiwa ofisa habari katika Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC). Ziara zote hizo zimenipa picha ya vyanzo vya migogoro.

Mojawapo ya vyanzo  hivyo ni kwa sababu baadhi ya matajiri na vigogo serikalini wamenyakua mashamba makubwa vijijini, tena nyakati nyingine kwa kutumia njia haramu na hivyo kusababisha uhaba wa ardhi katika maeneo hayo.

Wakati mwingine ni kwa sababu Watanzania wengi wamekuwa na mazoea ya kuamini kwamba mashamba waliyoyarithi kutoka kwa wazazi wao ni mali yao halali na hivyo hawajawahi hata kuhangaika ili kupata nyaraka muhimu za kisheria.

Wakati mwingine maofisa ardhi na watendaji katika halmashauri wamekuwa wakipora ardhi baada ya kupokea hongo kutoka kwa watu wenye ukwasi mkubwa.

Lakini pia wakati mwingine viongozi wa serikali wamekosa uungwana na kuwandoa wananchi katika ardhi yao kwa kile kinachodaiwa ni kupisha miradi ya maendeleo. 

Walau baada ya kuona sababu hizo kwa uchache ni vyema kujadili nini hutokea baada ya kufumuka kwa hayo yote niliyoyataja hapo juu.

Jambo la kwanza ni uhasama wa wazi wazi ambao wakati mwingine huishia kwenye mauaji. Nilipata nafasi ya kutembelea wanavijiji katika mgogoro wa kugombea mashamba wilayani Mvomero.

Nilichokishuhudia ni uhasama na ukabila mkubwa ulioibuka kiasi kwamba usingeamini kwamba wanaogombana ni Watanzania wenzetu.

Kwa vile nilikaa mjini Morogoro kwa siku tatu mfululizo, nikiwahoji waathrika, viongozi wa serikali, waandishi wa habari na hata viongozi wa kiroho nilipata picha mbili kubwa juu ya mgogoro huo.

Kwanza ni kuzidiwa kwa serikali katika kutatua mgogoro huo, na pili ni pande husika za mgogoro kushindwa kuendana na matumizi sahihi ya ardhi ili kuendana na wakati tulionao. 

Nikianza na lile la kwanza nilipata fursa ya kumtembelea mkuu wa wilaya ya Mvomero kwa kipindi hicho mwaka 2013, Anthony Mtaka. Na Mkuu wa Mkoa Joel Bendera.

Kimsingi walieleza jinsi walivyojitahidi kuzuia mgogoro usipanuke zaidi na kusababisha mauaji makubwa kutokana na pande mbili za mgogoro kujiandaa kwa makabiliano zaidi wakitumia silaha za jadi.

Lakini wote mwisho wa siku walinijibu kwamba wasingependa kuliongelea zaidi suala hilo kwa sababu bado kulikuwa na shauri mahakamani kuhusiana na mgogoro huo, na hivyo kauli zao zingeonekana zinaingilia uhuru wa mahakama.

Kwa maana nyingine mahakama ilitumika tu kama chombo cha kutuliza mihemuko lakini yaelekea mwisho wa siku labda wahusika hawakuridhika na hukumu (iwapo imetolewa tayari) na ndiyo maana migogoro hiyo bado inafukuta.

Picha ya pili kama nilivyoeleza hapo awali ni uduni wa teknolojia kwa pande zote mbili, yaani wakulima na wafugaji pia. Kwa sasa dunia iliyoendelea imeachana na utegemezi wa mvua za masika, na badala yake watu wanalima ndani ya majengo yenye hali ya hewa bandia, ‘green houses’.

Vivyo hivyo wamechana na ufugaji wa kutembeza mifugo kwenye eneo kubwa la ardhi na badala yake mifungo huwekwa ndani ya ranchi na kuletewa chakula humo humo.

Kwa lugha nyingine iwapo tungekuwa tumefikia kiwango hicho cha maendeleo basi wakulima na wafugaji wangekuwa ni marafiki wakubwa badala ya kuwa maadui. Urafiki wao ungeletwa na ile hali ya kutegemeana.

Mfugaji angekuwa anategemea malisho yake kutoka kwa mkulima, na mkulima angekuwa anapata maziwa na nyama kutoka kwa mfugaji, hawa wangekuwa ni marafiki wa kudumu.

Kinyume chake kulingana na hali niliyoishuhudia mkoani Morogoro chuki ilipandikizwa na ukabila ndani yake, kukajengwa taswira kwamba wafugaji wa Kimasai ni watu hatari na wauaji.

Mkuu wa Mkoa Joel Bendera alieleza kwamba amefanya utafiti wa kutosha na kugundua kwamba jamii za wakulima na wafugaji ziliishi kwa amani kwa muda mrefu, na akasema Chifu Kingalu Mwanabanzi kiongozi wa kabila la Walugurue aliwagawia Wamasai eneo kubwa kwa ajili ya mifugo yao miaka mingi iliyopita.
Na akasema chuki ya sasa ni kiashiria tu kwamba kuna mabadiliko makubwa katika matumizi ya ardhi, au kuna wavamizi kutoka nje ambao wamesababisha mgogoro huo.

Je nini kifanyike sasa?
Njia sahihi ya kwanza ni kukubaliana na ukweli kwamba mabadiliko ya nyakati yanahitaji pia mabadiliko katika mambo hayo mawili, kilimo na ufugaji.

Kwanza, inabidi sasa wakulima waanze kutafuta mbinu ya kuhakikisha wanapata mavuno ya kutosha ndani ya ardhi hiyo hiyo waliyoimiliki kwa miaka kadhaa. Wanaweza kuhakikisha kwamba wao ndiyo wanakuwa chachu ya utunzani mazingira na hasa upandaji wa miti ili kuondokana na ukame.

Pili, siyo vibaya wakianza kuwa na hizo ‘green houses’ walau zinazotumia teknolojia ya mionzi ya jua ili kuhakikisha wanazalisha kwa kipindi cha mwaka mzima.

Na kwa upande wa wakulima wanatakiwa waachane na ufugaji wa mifugo mingi isiyo na tija. Badala yake wafuge katika eneo dogo na kuleta chakula cha mifugo yao ndani ya mazingira hayo hayo.

 Kwa upande wake serikali ambayo ndiyo imebeba dhamana kuu ya kulinda amani ihakikishe kwamba inawekeza zaidi katika eneo hilo la kilimo na ufugaji, na pia inawatafutia masoko ya uhakika wakulima na wafugaji ili wanufaike na kazi zao na kuondokana na umaskini.

Vyuo vya kilimo, asasi za kilimo, halmashauri za miji mbali mbali na hata vyombo vya habari vishiriki kikamilifu katika kubadilisha hali iliyopo sasa katika mfumo wa kilimo na ufugaji.

Serikali irejeshe uwiano wa umilikaji mali na hasa katika maeneo yote korofi ili kuondoa hofu na chuki miongoni mwa wakazi katika maeneo yafutayo: Loliondo, Mvomero, Mkomazi, Mbaralali, na hata Kilosa.
Viongozi wa kiroho, wabunge na madiwani washirikishwe kikamilifu katika kupata ufumbuzi wa suala hili.

0 comments:

Post a Comment