Listening to General Secretary Bankmoon addressing delegates from different countries on the theme of session

Having a lunch with other delegates from different countries day one at UN Geneva-Switzerland(Europe)

The storm ended in 2012. It was the day unspeakable, and the joy unforgettable at Chimwaga Hill Conference: The University of Dodoma-UDOM

With special attention while taking photos at American Embassy in Nairobi Kenya

With the smiling face in Nairobi Kenya at American Embassy :From the left is Dannilo from Mozambique, Anderson from Tanzania, Dr.Katabaro-Tz, and the blogger in the right side Dr.Msoline

Friday, 13 January 2017

Tupate funzo kutoka Sichuan kuhusu tetemeko la Kagera

Tupate funzo kutoka Sichuan kuhusu tetemeko la Kagera

HIVI karibuni nikiwa bado nje ya nchi nilisoma katika mitandao ya jamii malalamiko juu ya matumizi ya pesa za misaada kwa waathirika wa tetemeko la Kagera.

Katika hali ya utani wengi wakasema kwamba uamuzi wa serikali kwamba pesa za michango zitatumika kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu iliyoharibiwa na tetemeko ni sawa na kunywa ‘uji wa mgonjwa’.
Wengine wakakilinganisha kitendo hicho kwamba ni sawa na mzazi kupewa pesa ya zawadi amtumzie mwanawe kisha akaamua kuitaifisha yeye mwenyewe.

Tukiachana na hoja hizo zilizokuja katika mfumo wa utani tuangalie mantiki nzima ya jambo hilo. Nimeona kwamba ufumbuzi wa Jimbo la Sichuan baada ya tetemeko la mwaka 2008 linaweza kusaidia hapa Tanzania.

Kilichojiri ni kwamba watu 88,000 hadi 90,000 walipoteza maisha na wengine 15,000 kujeruhiwa vibaya katika tetemeko hilo na miundombinu yote ikaharibika.

Kinachovutia hapo ni jinsi ambavyo Serikali ya China ilivyoyapindua maumivu ya madhara ya tetemeko na kuwa kivutio cha utalii katika eneo ambalo liliathirika na tetemeko.

Kwa sasa kati ya mwezi Machi hadi Desemba wakati mwingine eneo hilo hutembelewa na watu wapatao elfu ishirini kwa siku (20,000) kwa ajii ya utalii. Watu hao ni kutoka China yenyewe, Japan, Korea na nchi nyinginezo duniani.

Kwanza kila jimbo linalounda Jamhuri ya Watu wa China (PRC) walipewa kipande cha kazi cha kutengeneza yale yaliyoharibiwa na tetemeko kama vile ujenzi wa hospitali, shule na nyumba za makazi.
Baada ya hapo ziliundwa asasi za kiraia zipatazo 150 ili kutafuta namna ya kuwasaidia waathirika wa tukio lile. Kwa sasa waathirika wote wamejengewa nyumba na wanapata ruzuku kwa mwezi.

Kulingana na maelezo niliyoyapata kutoka kwa wenyeji wetu watu waliokuwa wanapata kipato cha shilingi milioni mbili kwa mwezi (2,000,000) leo wanapata hadi milioni kumi kwa mwezi (10,000,000).

Kwa maana hiyo japo hatushabikii majanga lakini tetemeko hilo kwa namna moja au nyingine limeongeza kipato kikubwa kwa watu wa eneo hilo kutokana na biashara ya utalii. Ili kuwasaidia wananchi wa eneo hilo serikali ya China ilifanya yafuatayo.

Kwanza ni kujenga jengo la makumbusho ya tetemeko hilo ambalo leo hutembelewa na watu wasiopungua elfu mbili kwa siku (2,000). Pili ni kuwahimiza wananchi wa majimbo mengine ili watembelee eneo hilo ili kuongeza kipato cha wenyeji na kujionea mambo yalivyokuwa.

Majengo mengi ya zamani ya kifalme ambayo yalikuwa ni ya mbao na yalikuwa yamesahaulika leo yamefufuliwa kwa ajili ya kuvutia biashara ya utalii. Kutokana na mkakati huo kuna bidhaa nyingi zinazozalishwa na kuuzwa na wenyeji kwa watalii wa ndani na wa kigeni.

Katika jengo la makumbusho ‘museum’ kuna picha mbalimbali za wahanga wa tetemeko hilo, video na jinsi Serikali ya China ilivyojitahidi kuwasaidia waathirika wa tukio hilo. Ikiwamo magazeti yaliandika nini na kauli za viongozi walipotembelea hapo zimewekwa kwenye video.

Ndani ya jengo hilo kipo chumba ambacho ukiingizwa kuna mashine inayotumika kutengeneza tetemeko bandia ambapo kuna kila kilichotokea utakiona hapo, barabara zinakatika, magari yanapinduka na kelele za watu wakiomba msaada.

Miongoni mwa kumbukumbu ambazo watu hufika kwa ajili ya ibada kwa marehemu wote ni jengo la shule ambamo jumla ya wanafunzi na walimu 55 walifariki baada ya kuangukiwa na majengo ya shule hususani mabweni.

Tunaweza kuiga mambo hayo kwa  sababu Tanzania kuna vivutio vingi vya kihistoria lakini haijafanyika kazi nzuri ya kutosha ya kuvitangaza au kuviweka katika mfumo mzuri na kuvutia watalii wengi kwa mpigo.
Mfano halisi ni Tembe la Dk. Livingstone, Tabora, nisingependa kulizungumzia sana kwa sasa lakini miaka michache nilishuhudia kwamba jengo linavuja kiasi kwamba baadhi ya nyaraka zimechafuka.

Nikashuhudia pia kwamba hata kulikuwa na vinyesi vya popo. Ni dhahari kivutio kama hicho cha kihistoria kinahitaji ushirikishi mkubwa wa manispaa ya mji husika kama ya Tabora.

Lingekuwa jambo la maana kwamba walau ungepatika hata usafiri wa Bajaj kuelekea katika eneo hilo la Kwihara. Lakini vile vile wangekuwapo wasimuliaji wenye uelewa juu ya muunganiko wa makazi ya chifu Fundikira na Sekondari ya Tabora.

Watalii wanatakiwa kufahamishwa kwamba Serikali ya Kikoloni ilifurahishwa na ukusanyaji kodi wa Chifu Fundikira na himaya yake nzima na hivyo akazawadiwa shule kwa ajili ya watoto wake na watoto wengine wa machifu.

Ipo nyumba ya makazi ya chifu huyo iliyojengwa na wakoloni wa kijerumani ikifanana kwa kiasi kikubwa na nyumba za walimu Tabora Sekondari. Kwa bahati mbaya historia hiyo huwa haisimuliwi katika namna ya uhusiano wa jambo moja na jingine.

Usimuliaji wa historia hiyo pekee hautoshelezi bila kuwepo kwa miundombinu kuelekea kwenye eneo hilo la utalii wa kihistoria.

Mfano huu unaweza kulinganishwa na yale yaliyojiri Sichuan kwa sababu serikali iliona ugumu wa ujenzi wa miundombinu na viwanda kwa pamoja na hivyo ikatafuta urahisi kwa kuviboresha vivutio vya utalii kwanza.
Na kwa maana hiyo vivutio vya mikoa mbalimbali ni pamoja na historia za wamisionari waliofika katika maeneo husika katika kuhubiri injili au hata wafanyabiashara ya utumwa walivyotembea mwendo mrefu kwa miguu kutokea Kigoma na hatimaye kuishia lilipo leo Tembe la Dk. Livingstone.

Labda tofauti niliyoiona ni pale Wachina wanapokuwa wabunifu zaidi na kuweka mambo mengine. Kwa maana hiyo kwa Tabora ingehusu hata kuingia kwa zao la tumbaku na uwepo wa watemi maarufu kama Mirambo na Isike na kisha vijitabu vya historia hiyo vingeuzwa kwa watalii.

Mavazi ya wenyeji na mkanda wa video na picha kama zipo vinaweza kuwa sehemu ya kumbukumbu hizo. Njia nyingine ingekuwa ni jukumu la manispaa kupanda miti ya kuvutia katika eneo hilo, au hata maua ya kibiashara na hata kuhakikisha eneo hilo linatumika kwa burudani katika siku za sherehe mbalimbali.

Nikiurejesha mjadala wenye kwa yale yaliyotokea Kagera ni kwamba Watanzania wote kwa ujumla wanaweza kuchangia kwa njia nyingi ikiwamo kuweka vituo maalumu vya kumbukumbu ya tetemeko hilo na kuwepo na mchango wa hiyari kwa waathirika kwa watu wote watakaohudhuria katika eneo hilo.

Ninaufahamu mji wa Kagera nafahamu walau vivutio vya kihistoria ikiwamo Seminari Kuu ya Ntungamo. Kanisa Katoliki limewekeza katika maeneo kadhaa ikiwamo hoteli kubwa ya utalii ya Kolping na hata Sekondari ya Wasichana ya Rugambwa. 

Wahaya wanafahamika kwa umahiri wao wa kutengeneza senene ambao wanaweza kutunzwa kwa teknolojia za kiasili bila kuharibika na hata ngoma za jadi maarufu kama zilivyoenezwa na wasanii maarufu kama ilivyokuwa kwa Saida Karoli.

0 comments:

Post a Comment