Tukiondoa hofu tutapata busara!
MWANADAMU katika kila kizazi hutawaliwa na uelewa wa kiwango fulani ambao ama huupata kutokana na mazingira aliyomo, mapokeo au hata mfumo wa elimu uliopo katika jamii yake.
Kwa nchi zetu za Kiafrika jambo hilo limekuwa na athari kubwa mbili: kwanza, wapo wale ambao wana hofu ya kubadilika na wameendelea kuwa na hofu isiyo na uhakika, na pia wapo wale wanaoona kila kilichopo mbele yao hakifai na hivyo kinastahili kuondolewa.Hata kabla sijajikita rasmi katika mjadala wenyewe ni vyema niseme kwamba njia bora ni kuyapokea mapya yenye tija, na kisha kuyabakiza yale ya zamani yenye tija pia. Na kwa mantiki hiyo ni vyema kukiri kwamba kila upande una jema lake na una udhaifu wake pia.
Busara inatakiwa itumike katika kuchuja lipi linafaa kubakizwa na lipi linafaa kuondolewa. Uwepo wangu China kwa miezi kumi iliyopita umenisaidia katika kuunganisha mambo hayo mawili kinadharia na kimatendo pia.
Nitaanza kuyadadavua moja baada ya jingine kama ifuatavyo: kwanza ninapozungumzia hofu niliyoitaja siwezi kuizungumzia kama vile inaelea katika ombwe au angani, bali ni lazima niiweke katika muktadha wa nchi yangu niipendayo sana ya Tanzania.
Binafsi ninamshukuru Mungu kwamba niliikataa hofu hiyo au hofu bandia miaka mingi na sasa ninakula matunda ya kukataa hofu hizo bandia. Ni kwa sababu tayari nimepata busara na sasa ninaona ni muda mwafaka kuwasherehesha na wengine utamu wa busara hiyo.
Najua utamu huo unaweza kupokelewa kwa namna tofauti kutokana na falsafa zinazotuongoza kila mmoja wetu. Mimi furaha yangu ni kufanya kile kinachoupa raha moyo wangu na wala sijatanguliza suala la kupata pesa kutokana na kile ninachokifanya.
Watanzania tumekwama na mkwamo wetu ulianzia hapo hapo kwenye matamanio makubwa ya pesa na kusahau amali (values) zingine maishani. Nimelishuhudia hilo katika nyanja nyingi ikiwamo kwa wanasiasa na hata kwa wanahabari wenzangu.
Leo kumekuwapo na maandiko sehemu mbalimbali, iwe ni Afrika, Amerika, Ulaya na kwingineko vikizungumzia kitu kinachoitwa “muujiza wa China”, lengo likiwa ni kuzungumzia jinsi taifa hili kubwa lilivyopata maendeleo kwa kasi kubwa hususani katika kipindi kifupi cha miaka 15 iliyopita.
Ni dhahiri mbegu halisi za maendeleo haya zilianza miaka zaidi ya 30 iliyopita lakini matunda yake yalianza kuonekana miaka 15 iliyopita na ndipo kukawa na mshangao mkubwa sehemu mbalimbali duniani na hivyo kuanza kuvutia pia vyombo vya habari.
Siri kubwa ya muujiza huo unaozungumziwa haiwezi kuwa nyingine bali ni kuondoa hofu na kukubali mawazo ya wengine. Wachina walianza tabia hiyo ya kukubali mawazo ya wengine muda mrefu na kuyafanyia kazi na kisha yakazaa matunda.
Haina maana ninaunga mkono kila lililopata kupitishwa na Wachina bali najaribu kutoa somo kwamba na sisi tukukibali ya wengine na kuondoa hofu tutasonga mbele. Hofu kubwa ninayoilenga hapa ni ile ya kuamini kwamba kuna chama kimoja tu kinachoweza kuingoza Tanzania na vingine vyote vinaweza kuondoa ‘amani na utulivu’ vilivyopo.
Kwa hakika hiyo ni hofu bandia na ndiyo kiini cha mkwamo uliopo Tanzania. Badala yake wananchi wetu wameanza kulishwa fikra viporo kwamba kuna mtu mmoja mmoja ambaye anaweza kuitwa shujaa na akalikwamua taifa kutoka kwenye mkwamo uliopo, hizo ni ndoto za mchana kweupe!
Tabia ya Wachina kukubali mawazo ya wengine imewasaidia sana. Miongoni mwa mawazo hayo yaliletwa na Mabudha waliotoka India na kuja kueneza dini hapa ingawaje chimbuko hasa la Ubudha ni nchini Nepal.
Maandiko ya Ubudha yana kauli mbiu kubwa, “Ukiondoa hofu utapata busara” nami nimeridhika na falsafa hiyo nikaona kwamba ndiyo haswa kiwe kichwa cha habari cha makala yangu ya leo.
Taifa la China limejengwa kwa kuamini zaidi katika falsafa na fikra jadidi za watu makini. Miongoni mwao alikuwa Confucius ambaye aliamini katika kukusaya mawazo ya watu, kuyachuja na kisha kutumia yale yanayoonekana yanafaa na kuyaacha mengine.
Ukiachana na mawazo hayo ya Wabudha na Confucius Wachina wanaziamini fikra za Lao-Tzu, ambaye ni baba wa falsafa zinazoitwa Taoism au Daoism. Huyu alikuwa na fikra kubwa kwamba acha kila kitu kichipuke kwa wakati wake kwa sababu hiyo ndiyo haki asili.
Falsafa zote hizi hazina mantiki yoyote iwapo zitajadiliwa hewani bila kulinganishwa na mazingira halisi ya Tanzania.
Mwaka 1992 nchi iliruhusu rasmi kuwapo kwa mfumo wa vyama vingi. Lakini watawala waliokuwapo madarakani wakawajengea wananchi hofu kubwa kwamba hawana tatizo na mfumo ila hao waliojitokeza kwamba ni wana mageuzi.
Kipindi hicho nilikuwa Afisa Uhamiaji ninayo kumbukumbu nzuri jinsi sisi maafisa katika idara nyeti serikalini tulivyolishwa hofu kwamba nchi yetu imo katika hatari kubwa ya kunyakuliwa na maadui wa ‘amani na utulivu’.
Sehemu kubwa ya mafisa wenzangu walikubaliana na hofu hiyo lakini mimi nilibakia kuwa “Thomaso Mwenye Mashaka”. Niliweka shaka yangu wazi bila kificho na hata siku moja bosi wangu akanitamkia “tii amri au acha kazi, idara yetu inaendeshwa kwa amri!”
Kwa vile nilikuwa nimejaliwa karama ya ujasiri ambayo wengine huitafsiri kwamba ni kiburi nikamjibu bosi wangu kwamba “sitaacha kazi na wala si kila amri hapa ni halali” hatimaye ‘kiburi’ changu kilizaa matunda nikahamishwa kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Dar es Salaam (DIA) kwa wakati huo, sasa Julius Nyerere International Airport.
Nilipelekwa Mtwara mjini na bosi mmoja kutoka makao makuu ya idara alisikika akisema “acha aende Mahurunga akasikilizie mtandao wake huko!” Niliamua kuachana na kazi hiyo nikaenda kufundisha sekondari kwa miaka minane nikiwa huko nilisomea uandishi wa habari nikarejea jijini Dar es Salaam nikiwa mwanahabari.
Kabla ya kuacha ajira hiyo niliwashirikisha baadhi ya marafiki zangu ambao walinisihi na kunijaza hofu kwamba haijawahi kutokea afisa uhamiaji yeyote akaacha kazi hiyo na akabakia akiwa amesimama wote huadhirika vibaya.
Niliipinga hofu hiyo nikaachana na ajira ya Uhamiaji, na wenzangu hawakuwa na njia wakanifanyia sherehe ya siri tena “siri sirini” pale Masai Pub Kinondoni mwaka 1999, tukaagana kwa upendo.
Leo hii nimeishi kwa miezi 10 hapa China mahali ambako mitandao yenyewe ndipo inatengenezwa! Na wala siyo Mahurunga nilikotakiwa kupelekwa, ingawaje Mahurunga yenyewe ilikuwa ni mpakani na Msumbiji ambako walipelekwa maafisa ‘wakorofi’.
Leo hii maafisa hao hao walionitia hofu wamekuwa wakinipigia simu na kusema “andika andika ndugu yetu uliona mbali, hatuna njia tumekaribia kustaafu lakini yanayoendelea nchini yanatutia uchungu sana!”
Nimetoa ushuhuda huu ili Watanzania wenzangu tuondoe hofu na tuachane na hiyo “Mahurunga ya kifikra” inayolikwamisha taifa letu na tuweze kusonga mbele.
MUNGU IBARIKI AFRIKA, MUNGU IBARIKI TANZANIA!





0 comments:
Post a Comment